KOCHA NGORONGORO HEROES AAHIDI USHINDI

Kocha Kim Poulsen anayeinoa
timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 cha Tanzania (Ngorongoro Heroes)
ameahidi kikosi chake kufanya vizuri kwenye mechi dhidi ya
Sudan.
Akizungumza leo (Aprili 20 mwaka huu) kwenye mkutano na Waandishi
wa Habari, Poulsen amesema timu yake imejiandaa vizuri kwa mechi hiyo na kiu yao
ni kushinda.
Kwa upande wake Kocha wa Sudan, Azhari Osman El Tahir
amesema ingawa haifahamu vizuri timu ya Tanzania, lakini wamejiandaa kushinda
kwani kwa muda mrefu walikuwa hawajashiriki mashindano ya vijana ya
kimataifa.
Mechi hiyo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo
itachezwa kesho (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa
10 kamili jioni kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh.
15,000.
Sudan iliwasili nchini jana (Aprili 19 mwaka huu) ikiwa na kikosi
cha wachezaji 20, viongozi kumi na mwandishi wa habari mmoja kwa ajili ya mechi
hiyo ya kwanza kabla ya timu hizo kurudiana jijini Khartoum kati ya Mei 4, 5 na
6 mwaka huu.
Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Brian Miiro
atakayesaidiwa na Mark Ssonko, Lee Patabali na Denis Batte wote kutoka Uganda.
Ejigu Ashenafi wa Ethiopia ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba
15.
Fainali za Afrika kwa michuano hiyo zitafanyika Machi mwakani nchini
Algeria wakati za Dunia zitafanyika nchini Uturuki kuanzia Juni hadi Julai
mwakani. Katika fainali za Dunia, Afrika itawakilishwa na timu nne za kwanza
kwenye fainali za Algeria.
No comments:
Post a Comment